Tuesday, April 24, 2012

ELIMU TANZANIA

    Ongezeko la vyuo vidogo nchini limechangia kuleta maendeleo kwa Watanzania wengi.
Hilo linatokana na kwamba wenye taaluma husika hupata ajira na kupunguza idadi ya wasio na ajira nchini.
Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo cha Highridge Training kinachotoa elimu inayozingatia ubora.
Chuo cha Highridge kilianzishwa mwaka 2011 kwa lengo la kutoa elimu ya fani mbalimbali kama biashara, hoteli, utalii, teknolojia ya mawasiliano na kozi fupi fupi za matumizi ya kompyuta.
Chuo hiki kilicho chini ya Kennedy Chacha akisaidiwa na Thomas Mendo kimesajiliwa na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na sasa kiko mbioni kupata usajili wa kudumu kutoka NACTE.
Mkuu wa Chuo hicho, Kennedy Chacha, anasema hadi sasa Chuo kina wanafunzi 188 wa fani tofauti tofauti katika ngazi ya cheti na stashahada.
       Aidha, anasema pia kilishatoa wahitimu 57 ambao wameajiriwa katika mashirika na taasisi mbalimbali nchini.
Chuo hiki kinatoa mafunzo kwa kushirikiana na Community Concern Training Institute (CCTI) iliyoko Kenya inayotoa kozi za ushauri nasaha, usimamizi katika biashara na elimu ya awali kwa watoto ikiwa ni hatua mojawapo tangu chuo kilipoanzishwa mwaka mmoja uliopita.
Kwa kuwa vyuo vyote hufundisha kwa kufuata mitaala, Chacha anasema Highridge inafuata mitaala ya Veta katika ngazi ya cheti. Na katika mafunzo ya Teknolojia ya Mawasiliano chuo kinafundisha kwa kufuata mitaala ya Uingereza.
       Anasema kwa kiwango cha stashahada huwa wanafundisha kwa kufuata mitaala ya NACTE na kuongeza kwamba tofauti kubwa iliyopo katika mitaala inayotumika katika ufundishaji ni lugha.
Akifafanua zaidi anasema kozi zinazotolewa na Highridge kwa ngazi ya cheti huchukua miezi tisa na stashahada huchukua miaka miwili.
Chacha anasema mafunzo hayo yanatoa fursa kwa watu wa rika zote kusoma.
Anasema anayesoma katika chuo hicho ana uwezo wa kujiunga na chuo chochote nchini kwa sababu kinatambulika na Veta na Nacte.
       Chacha anakiri kwamba si watu wote wenye uwezo wa kumudu gharama za kulipia masomo lakini wamejitahidi kutoa muda katika suala la ulipaji ili kuwasaidia kwa njia hiyo.
Mbali na hayo, pia chuo kimewai kutoa ufadhili kwa wanafunzi sita ambao hawakuwa na uwezo wa kumudu gharama za masomo ikiwemo yatima.
Anakiri elimu inayotolewa chuoni ina ubora na inakidhi soko la ushindani wa ajira sawa na elimu inayotolewa katika vyuo vikubwa nchini.
        Chacha anatoa wito kwa mashirika na taasisi kutowazingatia wahitimu waliotoka kwenye vyuo vikubwa pekee kuliko wale waliotoka vyuo vidogo.
Akizungumzia tofauti kati ya Highridge na vyuo vingine anasema inatokana na kuzidiana kitaaluma kwani wao wana walimu makini.
Aidha, utofauti mwingine mkubwa uliopo mbali na suala la taaluma ambalo ndio la msingi hasa ni ule utaratibu wa wanafunzi kuvaa sare.
       Anasema sare zinawaweka wanafunzi katika namna moja ya mfanano.
Mbali na hilo, Chacha anakiri kuwepo kwa ongezeko la vyuo vidogo nchini lakini anaona kwamba ni jambo zuri maana inaonesha ni jinsi gani watu wanavyotambua umuhimu wa elimu na kuwekeza katika sekta hiyo nyeti.
Anasema hilo linatokana na kuwapa fursa ya kusoma wale wasio na sifa ya kuendelea na elimu ya juu pindi wamalizapo elimu ya sekondari.
       Chacha anasema vyuo vidogo vinatoa fursa na kuwajengea msingi wa awali wale wasio na sifa na kuwa daraja kwa ajili ya kuwavusha kuelekea kwenye elimu ya juu.
Akizungumzia changamoto zilizopo miongoni mwa vyuo vidogo Chacha anasema baadhi yake vimekuwa vinatoa elimu nje ya utaratibu.
Chacha anasema vingi vinaendeshwa kinyemela na kusababisha kuharibu sifa ya vyuo vidogo makini.
Anafafanua kwamba dhana iliyojengeka miongoni mwa watu wengi hapa nchini ni kwamba vyuo vidogo ni vya kitapeli na elimu inayotolewa haikidhi ubora wa soko la ushindani wa ajira.
Chacha akifafanua zaidi hilo anasema tuhuma hizo zinaweza kuwa kweli au si kweli kwasababu inategemea na elimu inayotolewa na na chuo husika.
       Changamoto iliyopo kwa vyuo hivyo Chacha anasema ni muitiki mdogo wa watu kujiunga na vyuo vidogo kwa sababu wengi wanavidharau.
Akizungumzia changamoto iliyopo chuoni hapo anasema ugumu wa wanafunzi kuelewa kutokana na misingi mibovu ya kielimu waliyojengewa kwenye shule walizotoka.
Katika hilo wanajitahidi kuwajenga wanafunzi wao ili waondokane na changamoto hiyo.
Aidha, amelalamikia suala la tatizo la umeme nchini ambalo kwa kiasi kikubwa linawaathiri hasa wale wanaochukua mafunzo ya Teknolojia ya Mawasiliano.
Chacha anatoa ushauri kwa mamlaka husika zinazotoa usajili wa vyuo kutoweka ukiritimba katika mambo yanayohusiana na usajili wa vyuo nchini.
                       by JUMA MAYASA 12029

No comments:

Post a Comment