Tanzania: Taifa la ombaomba hadi michezoni | ||||||||||||
Ni msamiati wa kawaida sana katika medani ya michezo nyumbani Tanzania; kutembeza bakuli! Maana yake hapa ni kuwa ombaomba. Baada ya serikali yetu kuwa kinara wa kutembeza bakuli kwa wahisani, sasa michezo nayo imefuzu katika kufuata nyayo; kutembeza bakuli Ipo mifano kadhaa walau ya hivi karibuni. Chama cha Mpira wa Pete Tanzania (Chaneta) kinajiandaa kwa Mashindano ya Afrika. Tayari bakuli limeanza kutembea kila kona likibisha mlango wa maskini na tajiri kuomba mchango. Bila bakuli, mashindano hakuna na timu yetu haitashiriki Timu niipendayo kuliko zote Tanzania, timu ya soka ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), nao wanatembezewa bakuli hivi sasa wakijiandaa na mashindano yaliyo mbele yao. Kwao Twiga Stars kutembezewa bakuli limekuwa ni jambo la kawaida. Twende kwenye kikapu. Huko ni kichefuchefu zaidi! Timu za kikapu za jiji la Dar es Salaam (Dream Teams) zinajiandaa na mashindano ya majiji (Inter-Cities) ambayo mwaka huu yatafanyika nchini Uganda. Ukata umetanda kambini, wachezaji wanakwenda mazoezini kwa pesa yao mfukoni, kila mchezaji na vifaa vyake, na haijulikani kama nauli ya Kampala itapatikana au la, achilia mbali posho. Bakuli linatembezwa sasa Timu ambayo imekuwa nyanya kila siku lakini yenye bahati ya kupata ufadhili mnono katika miaka mitano iliyopita, Taifa Stars, mara kadhaa pamoja na udhamini wake imekuwa ikikosa kupata huduma kadhaa muhimu ikiwemo kuweka kambi kwa muda wa kutosha, kuwaita wachezaji wote wanaosakata gozi nje na kuwalipa posho stahiki, ama kuweka kambi katika hoteli yenye hadhi na sababu imekuwa ikidaiwa kuwa ni ukata Timu ya taifa ya ndondi inalia ukata, karate na Tae Kwon Do mambo ni hayo hayo. Mpira wa mikono, wavu na magongo sidhani hata kama inaendelea tena kuchezwa Tanzania, kama ipo basi timu zote zitakuwa za majeshi. Kwa ujumla hakuna penye ahueni, kila siku na kila mchezo ni ukata kwa kwenda mbele na suluhisho pekee Kwa viongozi wetu wa michezo, ni kutembeza bakuli. Lakini siwalaumu sana viongozi wetu wa michezo kwa kutegemea mabakuli na kuwa omba omba kama �Matonya� kila siku. Ni ka-utamaduni walikokarithi kutoka kwenye serikali yetu ambayo laiti tungekuwa na mashindano ya kimataifa ya kutembeza mabakuli, basi Tanzania ingetwaa dhahabu kila mwaka! Na sasa maji yanafuata mkondo. Ukiona tabia hii imeota mizizi katika sekta yoyote ile, tambua kuwa hapo kupata maendeleo ni sawa na ngamia kupenya mwenye tundu la sindano. Tusahau maendeleo iwe kwenye ndondi, riadha, soka, netiboli au kikapu kwa mchezo huu wa kutegemea mabakuli. Lakini jambo la kujiuliza, hivi kweli hakuna njia mbadala ya kuepuka tabia hii ya kujiaibisha kila siku kugonga milango ya watu na kuomba? Mimi naamini njia mbadala zipo, tena nyingi, lakini mawazo mgando ya viongozi wa michezo Tanzania ndiyo sababu ya kupenda kuendekeza aibu hii. Chama cha Mpira wa Kikapu mkoani Dar es Salaam kwa miaka mingi ligi yake ilikuwa ikidhaminiwa na bia ya Kilimanjaro. Tangu jamaa hao wajiondoe, basi akili za viongozi wote wa BD zikawa zimeganda na wameshindwa kutafuta udhamini ama kupata njia ya kujitegemea hadi leo. Nakumbuka wakati ule kikapu kikiwa kikapu cha ukweli, enzi za akina Patrick Nyembera wa Pazi na akina Lotty Cheyo wa Vijana, nilikuwa nalipa fedha kuingia uwanjani kuangalia mechi, na Uwanja wa Ndani wa Taifa ulikuwa unajaa kwelikweli. Leo hii hakuna hata kiingilio na uwanjani hakuna watazamaji tena, mvuto umepotea kwa viongozi kukosa ubunifu wa kuuendeleza mchezo. Enzi zile wakati netiboli inachezewa kwenye uwanja uliofunikwa na mabati wa Relwe Gerezani nikiwa shule ya msingi hadi sekondani, nilikuwa natoka Mabibo hadi Relwe Gerezani kuhakikisha naingia kuangalia mechi kama sio �kupiga chabo� kwenye matundu ya mabati uwanjani hapo. Netboli ilikuwa netiboli kweli. Leo hii ovyooooo Chaneta imebaki kutimuana, kugombana na Chaneza na kuwa ombaomba wa kutupwa badala ya kutafuta mbinu za kujitegemea na kuvutia wadhamini. Vivyo hivyo, kwa michezo mingine niliyoitaja hapo juu, hakuna uliosalimika iwe soka, ngumi, riadha, wavu, mikono, baiskeli na mingineyo. Hivi kweli tutarajie maendeleo katika michezo nchini Tanzania kwa kutembeza mabakuli? Jahazi la michezo Tanzania linazamishwa na viongozi wanaokosa ubunifu kama tulio nao sasa. Bila kuhakikisha viongozi hawa wanasafishwa wote bila kusalia hata mmoja, tusitarajie maendeleo ya aina yoyote katika michezo. Tutarajie ubia baina ya wanamichezo na ombaomba Matonya kuendelea kushika kasi kila kukicha. Kupata maendeleo michezoni kwa umatonya wetu wa kutembeza mabakuli, ni kuota ndoto za alinacha! |
The aim of the blog is to inform, entertainment, political issues, international and local news happening world wide
Tuesday, April 24, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment